Mwanza-Mhudumu wa Nyumba ya Kupumzikia Wageni wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Alipukiwa na Bomu


Damu zimetanda mbele ya lango la kuingilia Rest House ya Kanisa la KKKT Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria, mara baada ya tukio la kulipuka kwa bomu katika Ushirika wa Kanisa Kuu Imani jijini Mwanza

Juzi siku ya  Jumatatu tarehe 05.05.2014 majira ya saa 2 jioni,  bomu linalodaiwa kutegwa ndani ya  'Rest House' iliyoko katika  Kanisa Kuu Imani, Ushirika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria lalipuka na kujeruhi.
Kishindo kikubwa kilitokea na kutoa sauti kubwa na moshi huku kikisambaza misumari mingi midogo midogo na kumjeruhi vibaya mhudumu huyo hasa sehemu za miguuni na usoni.
Habari za kikachero zilizopatikana baadae  zilidai kuwa  Bomu hili lilitengenezwa kienyeji (local made). Bomu  hili  lilikuwa limefungwa  kwenye  kasha la kufungia Zawadi ( gift box) na kuwekwa kwenye mfuko mweusi wa plastiki  na kutelekezwa juu ya matupu ya soda yalokuwa kwenye   veranda ndani ya 'Rest House' hii.

Kwa mujibu wa maelezo ya Mhudumu wa 'Rest House' hii Bi Bernadeta Alfred (25) ambaye ndiye muhanga wa mlipuko huu, alisema kifurushi hiki kilichokuwa na bomu hilo kilikuweko  hapo juu ya makreti  ya soda tokea Jumamosi ya tarehe 3, Mei 2014. 

Siku hiyo ya Jumatatu saa mbili jioni ambayo mlipuko ulitokea muhudumu huyu Bi Bernadeta alitaka kujua  kilichokuwa kwenye kifurushi hicho hasa haada ya kuwauliza wenzake na kutompata aliyekuwa mmiliki wa kifurushi hicho. 

Maswali ya kina nini na kwa nini kimekuwa hapo kwa siku tatu yalimsukuma  kukifungua ili kubaini kilichokuwemo ndani.

Kwanza inadaiwa kuwa alikinusa na kusikia kinanukia udi. Harufu hii anavyodai ilimshangaza ikapeleka mawazo yake katika masuala ya kishirikina na kusita kukifungua.

Mara kilitoa moshi na ghafla akakiachia na ikawa kama nusura kwake kwani kingelipukia mikononi mwake ingekuwa hatari zaidi kwa maisha yake.

Mlipuko ulikuwa wa kishindo kikubwa uliotoa sauti kubwa na moshi huku ukisambaza misumari mingi midogo midogo iliyomjeruhi vibaya  muhudumu huyu sehemu za miguuni na usoni.

Hakukuweko na madhara  kwa majengo na  vifaa.

Muhudumu huyu wa 'rest house' hii Bi Bernadeta Alfred alikimbizwa  katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando ambako alifanyiwa upasuaji na amelazwa kwenye Wodi ya mifupa.

Uchunguzi wa nani na kwa nini wamefanya hivyo bado unaendelea. Mpaka sasa haijafahamika kama  lengo la wahusika  lilikuwa hilo ama bomu hilo liliachwa hapo baada ya lengo lao kushindwa.

Vyombo vya usalama  vinaendelea na kazi kubwa ya uchunguzi kubaini chanzo na wahusika wa tukio hilo. 

Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Valentino Mlowola akithibitisha tukio hilo, alisema kwamba uchunguzi wa awali uliofanywa na kikosi maalum kutoka Dar es salaam umebaini kuwa bomu hilo limetengenezwa kienyeji.

“Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili tubaini ni nani kafanya ili kama ni mtu au kikundi kimehusika tuchukue hatua haraka. Natoa wito kwa wananchi kutochukua vitu ambavyo hawana uhakika navyo, wanapoona vitu vya aina hiyo, watoe taarifa kwetu.” Alisema Kamanda Mulowola.

Kiongozi mkuu wa kanisa hili Rogath Lewis Mollel  ambaye ni Katibu Mkuu KKKT/DMZV amewaasa waumini wa kanisa hili na makanisa mengine kuacha kufikiri juu ya kulipiza kisasi kwani kisasi si kazi ya mwanadamu bali ni kazi ya Mungu peke yake na akawataka kushukuru na kuomba zaidi kuepushwa na hatari za namna hii.

"...hata sasa Bwana ametusaidia" 1Sam. 7.12b alinukuu mstari huu kutoka katika maandiko matakatifu.
Tunapaswa kujiuliza kuwa ni nani anayepanda mbegu hii hapa nchini na anafanya hivi kwa kusudio lipi na kwa faida gani?

Habari zaidi:
KKKT Watoa Tamko.

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki Ziwa Victoria, Andrew Gulle 
Alhamisi, 08 Mei, 2014.
KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria (DMZV) Ushirika wa  Imani, limeitaka Serikali kuhakikisha inawatafuta watu waliohusika na tukio la bomu lililolipuka kanisani hapo juzi Jumatatu tarehe 05.05.2014.

Pia, limewataka Wakristo kuwa watulivu, wasiogope wala wasitishwe na mashambulizi hayo na kwamba wasilipize kisasi.

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki Ziwa Victoria,
Andrew Gulle Akizungumza na wana Habari Ofisini Kwake.
Akizungumza kwenye Kanisa la Imani Makongoro Misheni jana, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki Ziwa Victoria, Andrew Gulle alisema wanaamini shambulio hilo ni la kigaidi na kwamba, Serikali inapaswa kuchukua hatua ya kuwasaka wanaohusika.

“Kanisa tunaamini tukio hili linahusiana na ugaidi, umefika wakati Serikali ikachukua hatua za kuwasaka waliohusika ili sheria ifuate mkondo wake,” alisema Gulle.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya dini wanasema huenda tukio hilo linatokana na migogoro inayoendelea kanisani hapo kwa sababu tayari kuna baadhi ya waumini wamejitenga kwa kuanzisha kanisa lingine.

“Wasikwepe matatizo yao ya ndani, kuna askofu aliuawa kwa kupigwa tofali kutokana na migogoro, hivyo hata hili (tukio) litakuwa ni migogoro inayoendelea,” alisema mmoja wa waumini ambaye hakutaka kutajwa jina lake.

Askofu Gulle alikanusha kuwapo kwa migogoro kanisani hapo na kwamba, tukio hilo halihusiani na mgogoro wowote ndani ya Kanisa bali ni ugaidi.

Hali ya majeruhi wa mlipuko wa bomu uliotokea kanisani hapo, Benadeta Alfred, imeelezwa kuendelea vizuri katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando alikolazwa.

 “Hali ya mgonjwa ni nzuri ukilinganisha na tulivyompokea kwani hata kuongea alikuwa hawezi, lakini hivi sasa anaweza kuongea japo kwa shida,” alisema Lema.





0 comments:

POLL

Which structure of government do you prefer to be implemented in Tanzania?
  
pollcode.com free polls 

TOA MAONI YAKO HAPA (NI BURE)

Name

Email *

Message *

Copyright © 2014 Hii Wiki jijini Mwanza