Fununu za Kuwanasa Walio Tega Bomu Arusha Night Park Bar Zapatikana.
Askai wakifanya doria eneo la tukio. |
Bomu hili lililojjeruhi watu wapatao 20, lililipuka ndani ya baa hii maarufu mkoani Arusha, Jumapili, Aprili 13, 2014 saa 1:30 usiku, wakati wateja wakiangalia mechi ya soka, Ligi kuu ya Uingereza, kati ya timu za Chelsea na Swansea
Taarifa toka vyanzo kadhaa zinadai kuwa tayari makechero wa polisi kwa kushirikiana na wale wa Idara ya Usalama wa Taifa wanachunguza sehemu ya matukio ya picha hizo, kabla na baada ya bomu hilo kulipuka.
Habari zinaeleza kuwa sehemu ya picha hizo zinaonesha watu wawili waliokuwa na mfuko mweusi wakiingia na kuweka mfuko huo katika moja ya sehemu za baa hiyo na muda mfupi baadaye mlipuko ukatokea.
Aidha kitu kinachodhaniwa pia kuwa ni bomu kiligundulika katika baa ya Washington iliyopo jirani na kituo kikuu cha mabasi madogo katikati ya jiji la Arusha siku hiyo hiyo, usiku wa saa tano.
Akizungumzia tukio hilo katika mkutano wake na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI) Isaya Mungulu alieleza kuwa makechero wanaendelea kuchunguza picha za kamera za usalama katika baa hiyo.
“Uwezekano wa tukio hilo kunaswa na kamera za usalama ni mkubwa sana na tunaweza kuwatambua wahusika hata kwa sura zao kwa sababu picha zinaonesha watu wawili wakiweka mfuko mweusi na baada ya muda mlipuko ukatokea,” alisema.
Alipotakiwa kusema nini kinafuatia kwa kupatikana kwa kielelezo kama hicho alikuwa na haya ya kusema.
“Ni kweli tumechukua matukio yote yaliyorekodiwa na kamera hiyo ya usalama lakini bado tuko katika hatua za mwanzo za uchunguzi wetu, hatuwezi kwa sasa kutangaza hadharani hatua tuliyofikia,”alisema Mungulu.
Kuhusu jeshi hilo kushindwa kuwakamata watuhumiwa katika matukio ya milipuko ya awali iliyotokea Arusha, Mungulu alisema. "Hata wahalifu na walioko nyuma ya matukio haya ni werevu na wana akili za kukwepa mkono wa dola, ila tutawatafuta na kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria pale tutakapowatia mikononi.".
Tukio la Jumapili ya Aprili 13,2014 saa 1:30 usiku ni la nne tokea kuwepo na kulipuka kwa mabomu hapo jijini Arusha.
Tukio la kwanza lilikuwa la bomu lililolipuka na kumjeruhi vibaya usoni aliyekuwa Katibu wa Bakwata Mkoani Arusha Abdulkarim Njonjo ambalo pia lilibainika kuwa ni bomu la kutengenzwa kienyeji.
Tukio la pili mwezi Mei mwaka jana bomu la mkono lilirushwa katika Kanisa Katoliki Parokia ya Olasit ambapo waumini watatu walipoteza maisha na wengi kujeruhiwa vibaya. Balozi wa Vatican nchini Askofu Fransesco Padilla na Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha Josephat Lebulu ingawa walikuwepo katika mkutano huu.hawakupata madhara yoyote.
Rejea tukio hili ambalo bado lko mwenye kumbukumbu za wengi.kwa njia ya video kama lilivyoripotiwa na ITV.
Tukio lingine la tatu ni la bomu kurushwa katika mkutano wa kampeni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika viwanja vya Soweto ambapo watu wanne walifariki dunia na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa.
Hadi sasa hakuna mtuhumiwa aliyekamatwa na hakuna kikundi chochote kile kilichowahi kutangaza au kudai kuhusika katika matukio yote haya.
Kinachotushangaza na kutupigisha butwaa ni kwamba ni kwa nini Arusha ambako nchi na mataifa yanapaona ni sehemu tulivu na yenye vivutio vya kitalii vingi kuwa eneo la shabaha kwa washambuliaji hawa?
Tunaomba uchunguzi uongezeke kuwabaini wahalifu hawa kwa kuliongezea jeshi la Polisi jijini Aruha nguvu za ziada toka Makao makuu ya Polisi nchini kwani hili sasa linapaswa kuchukuliwa kama janga la kitaifa.
0 comments: