Waziri Mkuu Mizengo Pinda Aitaka Familia ya Marehemu John Gabriel Tuppa Kuikimbilia Serikali Ifikwapo na Jambo.
Marehemu John Gabriel Tuppa Akiwa Kazini Enzi za Uhai Wake |
Ibada ya mazishi haya iliongozwa na Baba Askofu Mkude (Telesphor).
Akizungumza na waombolezaji Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema alimfahamu maerhemu Tuppa tangu mwaka 1993 pale alipoteuliwa kuwa mkuu wa wilaya.
Waziri Mkuu alielezea wasifu mfupi wa marehemu John Gabriel Tuppa kwa kusema.
"Marehemu Tuppa amekuwa mtumishi Serikalini kwa muda wa miaka 42 na katika muda wote huu, miaka 21 ya utumishi wake ameutumia akiwa Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa. Alikuwa ni mtu mwema aliyejali watu na wala hakuwa na tamaa za hovyo hovyo." Waziri Mkuu alisema .
"Kumpoteza mume na baba ni mtihani mkubwa lakini mkimtumaini Mwenyezi Mungu mtafaulu,"aliongezea. " Aliwasihi mjane wa marehemu na watoto wake kuwa wasisononeke wanapopatwa na jambo na wala wasisite kumwona Mkuu wa mkoa wa Morogoro, yeye binafsi ama Raisi Jakaya Kikwete kwa msaada zaidi.
Marehemu John Gabriel Tuppa amezaliwa tarehe 1 Januari, 1950, na katika enzi za uhai wake amewahi kuwa mkuu wa wilaya za Chunya,Mwanga, Bukoba,Muleba na Dodoma kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara mwaka 2011. Marehemu ameacha mke, watoto watano na wajukuu watano.
Mapema Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akitoa salamu za rambirambi alizozituma kwa Waziri wa Nchi,aOfisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa(TAMISEMI) Mhe.Hawa A. Ghasia kufuatia kifo hiki cha Mkuu wa Mkoa wa Mara Marehemu John Gabriel Tuppa alisema;
"Ni huzuni kubwa na pigo kubwa kwa serikali na hasa kwa watendaji wenzake mkoani Mara ambao alikuwa akifanya nao kazi." Taarifa ya rambirambi ilifafanua.
Marehemu Tuppa alifariki saaa 4.00 tarehe 25 Machi, 2014 katika Hospitali ya wilaya ya Tarime Kwa ugonjwa wa Shinikizo la damu.
Mapema kabla ya kifo chake kutokea Marehemu alitoka kufunga mafunzo ya askari wa jeshi la mgambo waliokuwa wakihitimu mafunzo yao katika kijiji cha Nyamwaga wilaya ya Tarime.
Katibu tawala wa mkoa wa Mara, Bw. Benedict Ole Kuyan, alisema "Bw. Tuppa kabla ya kifo chake leo asubuhi saa 4.00 akiwa na afya njema alifika katika ofisi ya mkoa na kuaga kuwa anakwenda kufunga mafunzo ya mgambo katika kijiji cha Nyamwaga wilayani Tarime," akaongeza kusema kwamba.
"Muda mfupi baada ya kufika katika ofisi ya mkuu wa wilaya, hali yake ilibadilika ghafla na alikimbizwa hospitali ya Tarime lakini alifariki wakati akipatiwa matibabu."
Akiongoza ibada ya mazishi,Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro,Mhashamu Telesphor Mkude aliwataka watu waliohudhuria mazishi hayo kufanya toba kama njia ya kuleta mabadiliko kwenye maisha yao.
"Ninawaomba kila mmoja mahala hapa afanye toba na kuwa mkweli na kuacha uchakachuaji...kila mtu kwa imani yake aache mabaya na kutenda mema kama ndugu yetu John Tuppa alivyojitoa kufanya kazi kwa ajili ya wengine,"Askofu Mkude alihimiza.
"Jihoji unaongozaje watu katika ofisi yako, katika ngazi mbalimbali, iwe wizarani, mkoani,wilayani hata kwa mtendaji wa kijiji? Je unawafanyaje watu katika biashara unayofanya?Je unawazalilisha kwa kuwauzia vitu vibovu? Je unawauzia madawa ya kulevia?"
Akamalizia kwa kuwataka watu wote kwa imani zao kuendelea kuombea mchakato wa katiba mpya ili tupate katiba bora zaidi.
"Tuna wajibu kama wacha Mungu kuwaombea wajumbe wa bunge maalumu la katiba ili waweze kuifanya kazi hiyo sawa na mapenzi ya Mungu.Tusipowaombea watafanya vitu vya ajabu," alishauri.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi (Mahusiano) Bw.Stephen Wassira akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya wabunge wa Mara alivunja mbavu waombolezaji waliokuweko mazishini aliposema.
"Baba askofu Mkude(Telesphor),ukiuliza hapa nani anataka kwenda peponi,wote hapa tutanyosha mikono.lakini tatizo ni masharti yanayoambatana na safari ya kwenda huko peponi. Kila mtu anaona ugumu wa hayo masharti ukiwemo na wewe Baba Askofu,"umati uliokuwepo ukaangua kicheko.
Mazishi haya yalihudhuriwa pia na Makamu wa Raisi Dk. Mohammed Gharib Bilal na baadhi ya mawaziri ,wabunge wa mkoa wa Mara na Morogoro,wakuu wa mikoa mbalimbali, viongozi wa dini na vyama vya siasa walikuwepo.
Chanzo: Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma.Jumapili,Machi ,30,2014
0 comments: