Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imepitisha uamuzi wa kutotahini tena mtihani wa somo la Dini kuanzia mwaka huu. Katika kupitisha uamuzi huo, Wizara ilikutana na taasisi za Kikristo pekee mwezi Machi mwaka huu na baadae kuwapa taarifa Bakwata juu ya maamuzi yaliyofikiwa. “Sisi tumefanya tu kupewa taarifa kuwa Serikali imepitisha uamuzi huo, lakini katika kujadili suala hilo hatukufahamishwa, Wizara ilikutana na wadau wa Kikristo pekee.” Amesema afisa mmoja wa Bakwata akielezea juu ya barua waliyoandikiwa na Kamishna wa Elimu juu ya uamuzi huo. Afisa huyo akasema kuwa wao kama Bakwata wameshangaa na kushtuka sana. Akasema kuwa pamoja na kuwa hawakushirikishwa wanakuja kupewa tu taarifa, lakini wanashangaa pia kwa sababu hata walipopewa taarifa na Kamishna wa Elimu, wameambiwa jambo hilo liwe siri.

Jambo hili linafanywa “SIRI, je Serikali inataka Waislamu wasiambiwe? Kwanini? Kuna agenda gani? Amehoji afisa huyo ambaye hata hivyo hakutaka kutaja jina lake akisema kuwa yeye sio msemaji wa Bakwata. Awali taarifa juu ya kikao cha Wakristo na Wizara juu ya mitihani ya dini, zilianza kuvuja kupitia kwa Wakristo waliohudhuria ambao walipokutana na wadau kutoka upande wa Waislamu waliwalaumu ni kwa nini hawakuhudhuria wakasaidiana kupinga uamuzi huo wa Serikali. Hata hivyo, wadau hao kutoka Islamic Education Panel waliwafahamisha wadau hao wa Kikristo kuwa wao walikuwa hawakupewa taarifa.

Kufuatia kuvuja kwa taarifa hizo, baadhi ya wajumbe wa Islamic Education Panel walifuatilia jambo hilo Bakwata wakidhani kuwa huenda Bakwata wao walipewa taarifa. Hata hivyo, maofisa wa Bakwata wakasema kuwa nao wanasikia tu, hawakualikwa. Kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikitahini masomo ya Dini ya Kiislamu (Maarifa ya Uislamu) na Kikristo (Divinity) katika mitihani ya kidato cha nne na sita na pia katika Mafunzo ya Ualimu ngazi ya Cheti na Stashahada. Kwa upande wa Maarifa ya Uislamu, Wizara imekuwa ikishirikiana na Islamic Education Panel katika kuandaa mihutasari na mitihani kwa ngazi zote hizo.

Vitabu vya mihutasari hiyo, kwa ngazi zote, katika jalada vimewekwa nembo ya Serikali na ile ya Islamic Education Panel na kusainiwa na Kamishana wa Elimu. Hata hivyo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, haikuwaita IEP katika kupitisha uamuzi huo mkubwa na wenye athari kubwa kwa vijana wa Kiislamu na vyuo vya Kiislamu. Hivi sasa Vyuo Vikuu kama kile cha Waislamu Morogoro (MUM), pamoja na wanafunzi wa kozi nyingine, huchukua wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na kufaulu Somo la Islamic Knowledge kwa ajili ya kuchukua kozi ya Sheria na Sharia kwa pamoja. Aidha, huchukua pia wanafunzi hao kwa ajili ya kozi ya Masomo ya Dini na Ualimu, yaani BA Islamic Studies and Education. Kwa upande mwingine, Chuo Kikuu cha Elimu Zanzibar (Chukwani) na kile cha Tunguu, navyo vinachukua wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na kufaulu somo la Maarifa ya Uislamu kwa ajili ya kozi zao mbalimbali. Vipo pia vyuo vikuu vya Mbale Uganda, Sudan, Uturuki, Malaysia na sehemu nyingine ambapo wana kozi zinazohitaji somo la Maarifa ya Uislamu kama vile Islamic Banking.

Kwa uamuzi huu wa Serikali, ina maana kuwa sasa itakuwa vigumu kwa MUM na Chukwani kupata wanafunzi wenye sifa kwa hiyo huenda vikalazimika kufuta kozi hizo. Hii maana yake ni kuwa uamuzi huu unapunguza idadi ya wanafunzi wa Kiislamu wanaokuwa na sifa za kupata elimu ya juu. “Kinachosikitisha ni kuwa Serikali imeamua kukaa na Wakristo pekee kupitisha maamuzi mazito kama haya bila kujali athari yake kwa vijana wa Kiislamu na taasisi za Kiislamu nchini.” Amesema mjumbe mmoja wa Islamic Education Panel akizungumzia suala hilo. “Hii ni dharau iliyopitiliza kiwango, Serikali inachukuaje maamuzi kama haya bila kujali kuwa kuna shule za Kiislamu na Vyuo vya Ualimu vya Kiislamu pamoja na Vyuo Vikuu ambavyo vinategemea kupata wanafunzi kutokana na wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita wenye somo la Maarifa ya Uislamu?” Amesema mjumbe huyo wa Islamic Education Panel ambaye hata hivyo hakutaka kutajwa jina lake gazetini.

“Kama Serikali imeona kuna mantiki kujitoa katika kutahini somo hili, kwa nini ifanye kinyemela? Kwa nini isiwashirikishe wadau husika ili kujua, ni utaratibu gani mwingine utafanyika ili vyuo vya Kiislamu vilivyopo visiathirike? Kwa nini wasikae pamoja na Panel? Mbona waliwaita Wakristo? Kitu gani kiliwafanya wakwepe kuwaita Waislamu, ni dharau, UDINI, au kuna agenda ya siri?”

Mdau mmoja wa Kikristo aliyekuwa katika kikao hicho cha Machi kati ya Serikali na wadau wa Elimu wa Kikristo alipoulizwa kuwa katika kikao hicho Serikali imetoa hoja gani ya kufuta mtihani huo alisema kuwa, hakuna jambo lililoelezwa la kujenga hoja madhubuti, lakini yeye binafsi anadhani ni kutokana na masuala ya Waislamu toka walipopinga matokeo ya Islamic mpaka ikabidi Baraza la Mitihani liyabadili. Wajumbe wa Islamic Education Panel wanasema kuwa, wakati Waislamu wametimiza matakwa yote ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya kuwa na Mihutasari na vitabu kwa ngazi zote, Wakristo hawakuwa wametimiza matakwa hayo, hawakuwa hata na mihutasari, lakini somo lao lilikuwa likitahiniwa.

Hata hivyo, akasema, hao hao ambao hawakuwa wametimiza matakwa ya Wizara na Baraza la Mitihani, ndio walioitwa kupitisha uamuzi wa Serikali kujitoa katika kutahini mtihani huo. “Waislamu wakilalamika kuwa kuna ubaguzi, udhalilishaji, uonevu na udini, wanaambiwa wanafanya uchochezi, hivi Serikali inaweza kukaa na Waislamu pekee na kufanya maamuzi makubwa yenye kugusa masilahi ya Kanisa Katoliki na Wakristo wote, halafu ifanye tu kuwapelekea taarifa Baraza la Maaskofu juu ya maamuzi hayo?” Alihoji. Wachambuzi wa masuala ya kidini na kijamii nchini wanasema kuwa huenda Serikali imeamua kujitoa katika suala hili ili ipate fursa ya kuweka mkakati mwingine wa kuibuka na somo la dini mseto baada ya kukwama huko nyuma. Hata hivyo wengine wanasema kuwa hii ni moja tu ya mikakati ya kupunguza idadi ya vijana wa Kiislamu wenye sifa za kujiunga na vyuo vikuu.

Wengine wakakumbusha kuwa zilipoanzishwa shule za kwanza za seminari za Kiislamu, Serikali ilitangaza kuwa shule hizo sio shule zinazotambulika. Ni Madrasa. Kwa hiyo wanafunzi wake wakimaliza kidato cha nne wasingepatiwa nafasi za kusoma kidato cha tano katika shule za Serikali. Na kwamba kwa wale watakaomaliza kidato cha sita, wasingechaguliwa kuingia vyuo vikuu na vyuo vingine vya Serikali. Kwa vile isingewezekana kutangaza kuwa wasiotakiwa ni Waislamu pekee, ilibidi tangazo liguse shule zote pamoja na seminari za Kikristo.

Hata hivyo, baadae alilazimka wenyewe kuondoa tena kimya kimya sera hiyo kabla haijafanyiwa kazi, baada ya kuona kuwa watakao athirika zaidi ni vijana wa Kikristo kwa sababu ni taasisi za Kikristo zilizokuwa na shule nyingi za seminari. Ni kwa sababu ya matukio kama hayo, baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa huenda kuna agenda ya siri inayowalenga Waislamu na ndio maana waliitwa Wakristo pekee ili waelimishwe kuwa wawe radhi kutoa muhanga mtihani wa ‘Divinity’. 

Kwa upande mwingine huenda hawakuitwa Waislamu kwa kuhofiwa kuwa wangehoji mambo ambayo yasingeweza kupatiwa majibu moja likiwa ni utaratibu gani umeandaliwa kuhakikisha kuwa MUM, Chukwani na vyuo vingine vya Kiislamu vyenye kozi za Islamic Studies, Shariah na Islamic Banking, vitapata wanafunzi kulingana na vigezo vya Mamlaka ya Vyuo Vikuu- Tanzania Commission for Universities (TCU). Habari kutoka ndani ya Bakwata na Islamic Education Panel zinasema kuwa taarifa kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi juu ya suala hilo, imeeleza kuwa nao Wizara wamefanya kupewa maelekezo na Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu.

Na kwamba Wizara ilitakiwa kukaa na wadau, kwa maana ya taasisi za kidini kuangalia suala hilo. Hata hivyo, haikuweza kufahamika kuwa uamuzi wa kutokuwashirikisha Waislamu na badala yake kukaa na Wakristo pekee, ilikuwa ni maelekezo kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi au ulikuwa uamuzi wa Kamishna wa Elimu. Wadadisi wengine wanasema kuwa jambo hili limetokea Baraza la Mitihani (NECTA) na kwamba kama ambavyo Baraza hilo liliona umuhimu wa kuajiri Mchungaji wa kutizama masilahi ya wanafunzi wa Kikristo na kugoma kuajiri Muislamu, ndio mtindo huo huo umetumika katika kuita kikao cha Wizarani. Kutokana na hali hiyo, Waislamu kupitia taasisi zao, wamepanga kumuona Katibu Mkuu Kiongozi kupata ufafanuzi juu ya suala hilo.

Na kwa kuwa suala hili linagusa masilahi ya Waislamu wote nchini, litafanyiwa taratibu za kujadiliwa na kupitishwa maamuzi ya pamoja. Hadi jana tukienda mitamboni juhudi za kuwapata wahusika Wizara ya Elimu na NECTA kuzungumzia suala hili, hazikuweza kufanikiwa.

0 comments:

POLL

Which structure of government do you prefer to be implemented in Tanzania?
  
pollcode.com free polls 

TOA MAONI YAKO HAPA (NI BURE)

Name

Email *

Message *

Copyright © 2014 Hii Wiki jijini Mwanza